Latest Updates

MZIMU WA MISS TANZANIA WAMTESA LUNDENGA

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa, imeiamuru Kamati ya Miss Tanzania, kurudisha zawadi kiasi cha Sh18 milioni alizoshinda Sitti Mtemvu kwa mshindi wa pili, ambaye ni Miss Tanzania 2014, Lilian Kamazima.

Maazimo hayo yalifikiwa jana wakati wa kuifanyia tathmini kamati hiyo, kazi ambayo iliwahusisha wadau kutoka wizarani, Basata, TGNP, wadau wa masuala ya sanaa na vyombo mbalimbali nchini. Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema chombo hicho kitahakikisha kinasimamia suala hilo mpaka Miss Tanzania 2014, Lilian Kamazima apate zawadi zake kwani ndiye mshindi halali.

“Utaratibu wa zawadi zote, baraza tunatakiwa kufahamu na mkanganyiko ambao ulikuwa umejitokeza, una sababu zake na ndiyo maana walisema kwamba wanalifanyia kazi kiofisi, tunaamini kwamba watafanya hivyo,” alisema na kuongeza:

“Uzuri wake ni kwamba ile Sh10 milioni iliyotolewa kama zawadi ya gari ndiyo atapewa kwa sasa kwani ni mwenye haki zote kama mshindi, lakini hii Sh8 milioni ambayo wao wanasema kwamba walishampa Sitti na kwamba wataifanyia kazi, tunahitaji wafanye hivyo ili apewe stahiki yake zote.”

Mkurugenzi wa Lino Agency, Hashim Lundenga alisema suala lililojitokeza mwaka huu lilikuwa nje ya uwezo wao, kwani cheti kilikuwa ni halisi kutoka Rita na ndiyo maana walimwamini Sitti, lakini warembo wengi wamekuwa wakidanganya umri.

“Watu tangu zamani walikuwa wanadanganya umri na mwaka huu tuliamua wote walete vyeti za kuzaliwa, hakuna mbinu nzuri ya kuzuia zaidi ya hiyo.”

0 Response to " MZIMU WA MISS TANZANIA WAMTESA LUNDENGA"

Post a Comment