Latest Updates

KWENU wauza sura katika video mbalimbali Bongo (video queens)

KWENU wauza sura katika video mbalimbali Bongo (video queens), najua mpo wengi lakini pengine labda niwataje wachache ambao mna majina makubwa; Agness Gerald ‘Masogange’, Rehema Fabian, Husna Maulid na Lulu ambaye umeonekana juzikati katika video ya msanii wa Bongo Fleva, Y-Tone, Shitobe.

Bila shaka mko poa na mnaendelea na maisha yenu ya kila siku. Mkitaka kujua hali yangu, mimi niko poa, naendelea na maisha yangu na kazi zangu kama kawaida kusahihisha wale ambao hawaendi kwenye mstari kama nyinyi.

Suala la nyinyi kurekodiwa picha za utupu limekuwa kama desturi. Mnarekodiwa video za utupu au kupiga picha za utupu kisha kuzisambaza (kusambazwa) katika mitandao ya kijamii.
Tena mara nyingi wanaowarekodi huwa wanakuwa ni wapenzi wenu, sijajua mnawaamini kuwa watatunza siri au vipi?

Dada zangu, hata kama mnapiga hizo picha kwa lengo la kupata umaarufu lakini niwaambie tu, mnajidhalilisha. Kwanza mnajidhalilisha nyinyi wenyewe, mnawadhalilisha wanawake wenzenu ambao wanawaona kwenye mitandao mbalimbali mkiuza utu wenu.

Nawasikitikia maana mnaonekana hamjitambui. Mmepewa maumbo mazuri, muonekano ambao mnaweza kuutumia katika tasnia ya urembo au hata utangazaji na mkapata fursa kibao za mafanikio. Badala yake mnaamua kujishusha thamani kiasi hicho.

Nani aliyewaroga? Elimu ya matumizi ya mitandao mbona inatolewa kila siku? Halafu mwenzako akinyolewa na wewe si unapaswa kutia maji za kwako? Haiwezekani tuliona kwa Masogange, Rehema, Husna bado tena kabinti kawatu kutoka Mbeya (Lulu) nako kakafanya hivyohivyo.

Mi sitaki kuamini kwamba zinavuja kwa bahati mbaya, tatizo langu linaanzia pale mnapojipiga au kukubali kupigwa. Mnajipiga au kupigwa za nini? Kuna faida gani kujipiga? Hakuna haja ya kujipiga utupu hata kama ni biashara bwana mbona mnaweza kupata biashara pasipo kujipiga picha za utupu.

Igeni mifano kutoka kwa nchi za wenzetu ambao wametangulia katika masuala ya urembo, miili yenu ni biashara lakini ishu inakuja tu kwamba mnaitumiaje? Kuna dili nyingi siyo lazima kujidhalilisha. Kuna dili za matangazo mbalimbali ambayo mnaweza kutumika kupamba mabango, mkaingiza fedha nzuri tu.

Kuna uigizaji, kuna utangazaji, kuna vitu vingi tu ambavyo kimsingi mtu ukiweka nia, hakika mnaweza kufanikiwa kupitia mwili wako. Hasara kubwa ambayo mtu unaweza kukumbana nayo katika mitandao, siku hizi ukishaingiza picha chafu basi itakugharimu maisha yako yote. Vizazi na vizazi vitashuhudia uchafu ulioufanya ukiwa kijana. Wanao na hata wajukuu wataweza kuona madudu yako uliyoyafanya kupitia mitandao, usikubali kurekodi wala kurekodiwa.
Kwa leo ni hayo tu.

SOURCE:GLOBAL PUBLISHERS

0 Response to "KWENU wauza sura katika video mbalimbali Bongo (video queens)"

Post a Comment