Latest Updates

WAGOSI WA KAYA WAPO KATIKA HATUA YA MWISHO KUKAMILISHA ALBAMU YAO
KUNDI la muziki wa Hip Hop kutoka Tanga Wagosi wa Kaya limerudi rasmi kwenye ulingo wa burudani ya muziki baada ya kuwa kimya kwa muda wa miaka 8. Kundi hilo linaloundwa na Fredrick Mariki a.k.a Mkoloni na John Simba a.k.a Dr John lenye makazi yake jijini Tanga na Dar es salaam lipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha album waliyoipa jina la “UAMSHO”.

Akiongea na Pro-24,Mkoloni alifafanua kuwa “Wagosi wa Kaya tunatarajia kufyatua album ya kihistoria baada ya kukaa kimya kwa miaka 8 na bado tumeona nafasi yetu ipo wazi kwa kile tulichokuwa tunakifanya kwenye gemu,”alisema Mkoloni.

Album hiyo ya UAMSHO inatarajiwa kuwa na jumla ya nyimbo 12 huku akiweka wazi baadhi ya nyimbo na wasanii walioshirikishwa,alizitaja nyimbo hizo kuwa ni pamoja Gahawa,Bao ambazo wameshazitoa sambamba na video zake na Tizauya kaya (tunarudi nyumbani) ambao wamemshirikisha Komando Lady Jay Dee,Thabit,Potofu,Unaaharibu,Kipo cha kuwaambia ambapo wasanii wengine watakaoshirikishwa ni pamoja na Prof Jay na wengineo.

Akielezea sababu za kuwashirikisha wasanii hao,Mkoloni alisema kuwa “Kitu ambacho watu wanapaswa kujua ni kuwa wasanii wengi tutakaowashirikisha ni wale ambao hatujawahi kufanya nao kazi tokea kuanza muziki na ni wasanii ambao wanaheshimika mbele ya jamii kutokana na uwezo wao wa kufanya kazi na ukaribu wao kwa jamii yetu”

Wagosi wa Kaya ambao kazi zao wamekuwa wakizifanyia katika studio ya Tongwe iliyopo Masaki jijini Dar es salaam hawakuweka wazi kama wamesaini lebo katika studio hiyo,”pale Tongwe rec sisi tunafanya kazi zetu hilo la kuhusu kuwa chini ya lebo kama lipo litafahamika kwani sisi ni watu wazima na hatuna tabia ya kuficha mambo”,alisema Mkoloni.

Kundi la Wagosi wa Kaya tokea mwaka 2001 mpaka sasa limeshaingiza sokoni album tatu ambazo ni Ukweli Mtupu mwaka 2002,Ripoti Kamili mwaka 2003,Nyeti mwaka 2005 na album ambazo hazikufanikiwa kutoka ni Tizauya Kaya mwaka 2005 waliyofanya Bongo Rec chini ya utayarishaji wake P Funk na X mwaka 2006 waliyofanya PKP chini ya utayarishaji wa Duke Tachez wa Tamadunimuzik,sasa huu ni mwaka 2014 ambapo jamii ya mashabiki wanasubiri album yao nyingine mpya inayoitwa UAMSHO kutoka Tongwe Rec.

0 Response to "WAGOSI WA KAYA WAPO KATIKA HATUA YA MWISHO KUKAMILISHA ALBAMU YAO"

Post a Comment