Latest Updates

UKATILI: Mke mjamzito akatwa mguu, amwagiwa tindikali

MJAMZITO_a17b4.jpg

Serengeti. "Ni zaidi ya miezi sita tangu nifanyiwe ukatili na mume wangu na mama mkwe. Nahangaika kuuguza mguu niliokatwa kwa panga kunyunyiziwa maji ya betri. sijui kama utapona. Kichanga nacho kinasumbua, jamani nimekosa nini mimi kwa Mungu."
Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio. Maneno ya ya Anna Sabai (20) mkazi wa Kitongoji cha Manyata Kijiji cha Nyamakendo Kata ya Mbalibali, wilayani Serengeti, ambaye anapaza sauti kutaka kujua walipo wanaharakati ambao kwa hali aliyonayo , angeweza kupata msaada kutoka kwao.
Ukatili aliofanyiwa Anna, mama wa watoto wawili katika ndoa yake na Hamisi Sabai (20) yenye migogoro na ambayo inazidi kuuweka Mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya kutokana na uwingi wa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
Agosti Mosi, 2013 ikiwa ni siku ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika mnadani, Anna akiwa na uja uzito wa miezi tisa na akihesabu siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na mume wake kwenda kuchunga ng'ombe, bila kujali hali yake.
"Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana," anakumbuka Anna wakati anaongea na Mwananchi kuhusu ukatili dhidi yake. "Nikiwa malishoni nilikaa chini ya kivuli huku ng'ombe wakiendelea kula majani. Hali ilivyozidi kuwa mbaya nilisinzia. Alipokuja mume wangu akanikuta nimelala na hapo hapo akaanza kunishambulia kwa kipigo, akidai kuwa nilikuwa na mwanamume kutokana na mapenzi kunoga ndio maana nilisinzia na kuacha ng'ombe wanazagaa."
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake, walipofika nyumbani mama mkwe wake Bhoke Sabai alizidi kumtia hasira kijana wake akidai kuwa nilikuwa na mwanaume, natakiwa kupewa kipigo ili iwe fundisho.
"Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea, bado akaona aache fimbo na akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto," anasema Anna huku akitokwa na machozi.
"Niliumia sana... nikatamani kufa, maana hali ilikuwa mbaya. Sikuwa na msaada. Baadaye akanifungia ndani ili watu wasijue; wala hakuna kwenda kutibiwa."
Amwagiwa tindikali ili kuzuia damu isitoke
Huku akiwa amebeba mtoto wake na kutembea kwa shida, Anna anasema ili watu wasijue unyama aliotendewa, walileta maji ya betri na kumwagia kwenye kidonda.
"Maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua. Nilifikia hatua kama ningepata kitu cha kujimaliza, ningejiua. Nilikuwa nasumbuliwa na mimba na huku naumizwa hivi," analalamika. "Jamani wanaharakati wanaotetea wanawake wako wapi maana nitakatwa mguu hivi hivi."
Anasema matokeo yake mguu ukaoza kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu na kwamba ndugu zake hawakuambiwa na mama mkwe wake alikuwa akiendelea kumkejeli kila wakati.
"Sijaona watu wenye roho ya kikatili kama hao, kwa kuwa walilenga kuniua bila kosa," anasema.
Aokolewa na mama yake mzazi
Anasema kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani ili majirani wasijue, kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu, kwa nini afe bila ndugu zake kumwona. Ndipo bila kutarajia alishtukia mama yake mzazi, Mnanka Chacha (48) akifika hapo baada ya kutaarifiwa na majirani.
"Nilipomwona mama nikasema basi sasa hata kama nikifa, niko katika mikono salama kwa kuwa huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu. Nilijua kama ningefia mkononi mwa hao huenda maiti ingetupwa kama mbwa. Nilijisikia ahueni kwa kumuona mama," anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu
Anasema kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha Hospitali Teule ya Nyerere kwa ajili ya matibabu na madaktari walipomwona walimwambia kuwa hawana uwezo tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo. Hivyo wakamwandikia barua kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.
Akosa pesa
Kutokana na ukata wake, alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi nyumbani kwake kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema, ili aweze kwenda naye Mwanza kwa ajili ya matibabu.
Mume achana barua ya rufaa
Katika kuhakikisha juhudi za kupelekwa hospitali hazizai matunda, akiamini kuwa mume wake alikuwa ameishajirudi, alimpa barua ya rufaa ili watafute fedha za matibabu, lakini yeye akaichana na kumuacha asijue la kufanya.
"Alichana barua ya rufaa ikawa sina namna yoyote ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Ikabidi nikae tu nyumbani nikiangalia mguu wangu unaoza. Kwa kweli nahitaji msaada kwa watu wanaoguswa maana kula yangu na hata ya mtoto ni ya shida. Siwezi kwenda zaidi ya hapa," anasema.
Anabainisha kuwa mumewe alichana barua kwa madai kuwa nimetoa siri polisi na kwa watu wengine na ndio maana akaamua kumkomoa kwa kuichana ili kupoteza ushahidi.CHANZO DJ SEK

0 Response to " "

Post a Comment